Serikali ya Ecuador imekiri kwamba ilimzimia mwanzilishi wa mtandao wa WikiLeaks Julian Assange huduma ya mtandao kwa muda.
Bw
Assange amekuwa akiishi katika ubalozi wa Ecuador jijini London tangu
2012 kukwepa kukamatwa na kupelekwa Sweden akajibu mashtaka ya
unyanyasaji wa kingono.Kupitia taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Ecuador hata hivyo imesema hatua hiyo haikutokana na shinikizo kutoka kwa Marekani.
WikiLeaks awali ilikuwa imeituhumu Marekani kwa kujaribu kuishurutisha Ecuador kuzuia mtandao huo wa ufichuzi usichapishe nyaraka za siri kuhsuu mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imekanusha madai hayo na kusema si ya kweli.
Ecuador imesema uamuzi wa WikiLeaks wa kuchapisha nyaraka ambazo zinaweza kuathiri mwelekeo wa uchaguzi Marekani ni wajibu wa mtandao huo.
"Ecuador huwa haichukui hatua ktokana na shinikizo kutoka kwa nchi nyingine," taarifa hiyo ilisema.
WikiLeaks awali ilisema Ecuador ilimzimia Assange huduma ya mtandao Jumamosi jioni.
Mtandao huo umekuwa ukifichua nyaraka za maafisa wa kampeni wa Hillary Clinton, zikiwemo barua pepe za mwenyekiti wake wa kampeni John Podesta.
Jumamosi ilitoa nakala tatu za maadhishi ya hotuba za kulipiwa ambazo Bi Clinton alizitoa katika mikutano ya Goldman Sachs.
Bi Clinton amekuwa akisema udukuzi unafanywa na watu kutoka Urusi.
WikiLeaks imefichua maandishi ya hotuba za Hillary Clinton katika mikutano ya Goldman Sachs
Kwenye barua pepe za majuzi zilizofichuliwa, Bi Clinton aliambia kongamano la Goldman Sachs kwamba angependa kuingilia kati hali Syria kisiri.
Alisema hayo akijibu swali la Lloyd Blankfein, afisa mkuu mtendaji wa benki ya Goldman Sachs mwaka 2013, miezi kadha kabla yake kuacha majukumu yake kama waziri wa mambo ya nje.
Published by Snackwells Media Group